Karibu katika Jarida Toleo namba Tatu la Kiswahili la Mpango wa kuimarisha vijana kufikia malengo yao kiafya na kimaendeleo (SYP).
SYP ni mpango wa kimageuzi uliozinduliwa mwaka 2013 kwa nchi za Kusini mwa Afrika ambazo ni Botswana, Eswatini, Lesotho, Malawi, Namibia, Afrika ya Kusini, Zambia na Zimbabwe. Tanzania ilizindua rasmi mpango huo mnamo Aprili 2022. Kimsingi, mpango wa SYP umejikita katika kuboresha afya na ustawi wa vijana wa rika balehe kati ya wenye umri kati ya miaka 10 - 24.
Nchini Tanzania, mpango wa SYP unalenga mikoa inayopambana na viashiria duni vya kijamii, afya ya uzazi na haki za vijana wa rika balehe ikiwa ni pamoja na mimba za utotoni, VVU, ndoa za utotoni na ukosefu wa usawa wa kijinsia. Lengo kuu la mpango huu ni kusaidia jitihada za kuboresha afya na ustawi wa vijana wa rika balehe na vijana. Mpango wa SYP unamfumo wa uongozi na utawala uliokubaliwa na Serikali ya Uswisi ambayo inashirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA) katika kufadhili mpango huu.
Ndani kurasa za jarida hili la toleo la tatu, utaweza kusoma kwa kina mafanikio ya vijana kutoka mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Kigoma na Shinyanga. Mafanikio haya yanaonyesha matokeo chanya ya mpango wa SYP, yakielezea kwa kina uzoefu wao kuhusiana na afya ya uzazi na haki za vijana, ujasiriamali, uongozi, na kupinga unyanyasaji wa kijinsia.
Mpango wa SYP ni kichocheo cha mabadiliko chanya, unakuza uelewa na utetezi wa vijana kupitia midahalo shirikishi inayosisitiza uwekezaji kwa vijana. Kupitia juhudi za mpango huu, vijana wana elimu kamili ya kijinsia na namna ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya kijamii. Hii inawawezesha vijana kufanya maamuzi sahihi kuhusu maisha yao.
Tunatumaini utafurahia kusoma na kushuhudia safari ya kustaajabisha ya vijana vinara ambao wameshawishi na kuhamasisha jamii zao, na kupelekea kuwa vinara wa mabadiliko.
Tunakualika katika safari hii ya kutia moyo na kusherehekea shauku ya vijana wanaojitahidi kuunda ulimwengu bora, na sahihi kwa ajili yao na wale wanaowazunguka. Kwa pamoja, tuunge mkono maono ya Mpango wa SYP na kuhakikisha kwamba malengo ya kila kijana yanatimizwa.